Kikosi cha Msaada wa Haraka cha Sudan (RSF), kinachoongozwa na Mohamed Hamdan Dagalo, Jumatano kilikaribisha juhudi za upatanishi za nchi jirani ya Sudan Kusini ili kumaliza mapigano yaliyodumu kwa mwezi mmoja na Wanajeshi wa Sudan (SAF).
Akiongea na wanahabari mjini Juba, nchini Sudan Kusini, Youssef Izzat al-Mahri, mshauri wa kisiasa wa RSF, alisema wako tayari kutekeleza usitishaji mapigano katika makubaliano yaliyofikiwa Mei 11 na SAF katika mji wa pwani wa Jeddah, Saudi Arabia.
Licha ya pande mbili zinazozozana kutia saini Azimio la Kujitolea Kulinda Raia wa Sudan ili kuwezesha uwasilishaji wa misaada ya dharura ya kibinadamu na kuhakikisha uokoaji salama wa raia, mapigano makali pamoja na mashambulizi ya anga na mizinga yanaendelea huko Khartoum, mji mkuu wa Sudan.
Hata hivyo Bw. Izzat alikanusha shutuma kwamba RSF inatumia raia kama ngao katika mapigano makali yanayoendelea na jeshi la Sudan tangu Aprili 15, na kuongeza kuwa RSF imekuwa ikilinda balozi za kigeni na kuwasaidia raia wanaoondoka Khartoum.