Rais Xi Jinping na viongozi wa nchi tano za Asia ya Kati wakutana na wanahabari kwa pamoja
2023-05-19 14:48:34| cri

Mkutano wa Kilele kati ya China na Asia ya Kati umefanyika kwa mafanikio leo Mei 19 katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa mjini Xi’an mkoani Shaanxi.

Rais Xi Jinping wa China na wageni wake ambao ni Rais wa Kazakhstan Kassym-Jomart Tokayev, Rais wa Tajikistan Emomali Rahmon, Rais wa Kyrgyzstan Sadyr Japarov, Rais wa Uzbekistan Shavkat Mirziyoyev na Rais wa Turkmenistan Serdar Berdimuhamedov wamekutana na wanahabari kwa pamoja.

Rais Xi amesema, yeye na viongozi hao wamesaini Azimio la Xi’an la Mkutano wa Kilele wa China na Asia ya Kati, na kupitisha matokeo yaliyopatikana kwenye mkutano huo, hatua zilizoweka dira kwa maendeleo ya uhusiano kati ya China na Asia ya Kati katika siku zijazo.

Rais Xi amesisitiza kuwa, ili kukabiliana na mabadiliko makubwa ambayo hayakushuhudiwa katika miaka 100 iliyopita, na kulinda maslahi ya kimsingi na mustakbali mzuri wa watu wa nchi mbalimbali, yeye na viongozi wa nchi tano za Asia ya Kati wamedhamiria kuungana mkono na kusimama bega kwa bega kwa ajili ya kujenga jumuiya iliyo karibu zaidi na yenye hatma ya pamoja kati ya China na Asia ya Kati, na kuchangia nguvu zao katika kusukuma mbele ujenzi wa Jumuiya ya Binadamu yenye Hatma ya Pamoja.