Rais wa Syria awasili Saudi Arabia kuhudhuria mkutano wa kilele wa 32 wa Jumuiya ya Nchi za Kiarabu
2023-05-19 22:08:17| cri

Rais wa Syria Bashar al-Assad amewasili Jeddah, mji wa magharibi mwa Saudi Arabia, ili kuhudhuria mkutano wa kilele wa 32 wa Jumuiya ya Nchi za Kiarabu unaofanyika leo Ijumaa mjini Jeddah.

Hii ni mara ya kwanza kwa rais wa Syria kualikwa kuhudhuria mkutano huo tangu mgogoro wa Syria ulipotokea mwaka 2011, pia ni mara ya kwanza kwa rais Bashar al-Assad kufanya tena ziara nchini Saudi Arabia baada ya miaka hiyo 12.

Tangu mgogoro wa Syria ulipotokea mwaka 2011, Jumuiya ya Nchi za Kiarabu ilisitisha uanachama wa Syria katika jumuiya hiyo, na nchi nyingi zilifunga balozi zao nchini Syria. Tarehe 7 Mei mwaka huu, Jumuiya hiyo iliitisha mkutano maalumu wa mawaziri wa mambo ya nje, na kuamua kurejesha uanachama wa Syria katika Jumuiya hiyo.

Katibu mkuu wa jumuiya hiyo Bw. Ahmed Aboul Gheit amesema hatua hiyo haimaanishi kuwa nchi zote za kiarabu zitarejesha uhusiano na Syria, bali ni nchi wanachama zitaamua zenyewe kama zitarejesha uhusiano na nchi hiyo au la.