Walinzi wa amani wa Umoja wa Mataifa wawadhibiti waasi wenye silaha kwenye vijiji kadhaa mashariki mwa DRC
2023-05-19 08:49:45| CRI

Naibu msemaji wa Umoja wa Mataifa Bw. Farhan Haq, amesema askari wa tume ya kulinda amani ya Umoja wa Mataifa nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (MONUSCO) wamewatimua waasi wenye silaha kwenye vijiji kadhaa vya eneo la Djugu katika jimbo la Ituri mashariki mwa nchi hiyo.

Bw. Haq amewataja waasi hao kuwa wanachama wa kundi la CODECO, ambalo ni muungano wa vikundi vya wanamgambo.

Bw. Haq amesema walinda amani wa MONUSCO, pia walishirikiana na jamii zinazozunguka eneo la Djugu, hasa wakimbizi wa ndani na viongozi wa vijana kukabiliana na waasi hao.

Mbali na hilo, Jumatatu iliyopita mjumbe maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Bibi Bintou Keita alitembelea eneo la Kalehe katika jimbo la Kivu Kusini kuona uharibifu uliosababishwa na mvua kubwa iliyonyesha hivi karibuni na kusababisha mafuriko makubwa, na kufanya watu zaidi ya 450 kufariki dunia.