Tanzania inataka kutumia fursa ya uhusiano wake mzuri wa muda mrefu na China ili kuvutia watalii zaidi wa China. China ambayo kwa sasa ndiyo chanzo kikubwa zaidi cha watalii duniani, watu wake wapatao milioni 150 wanasafiri kila mwaka kutembelea maeneo mbalimbali duniani.
Tanzania inapokea sehemu ndogo tu ya watalii kutoka China, huku Bodi ya Utalii Tanzania (TTB) ikitabiri kuwa karibu watalii 45,000 kutoka China wanatarajiwa kutembelea Tanzania hadi mwishoni mwa mwaka huu.
Waziri wa Maliasili na Utalii Tanzania Bw. Mohamed Mchengerwa, amesema anataka juhudi zaidi zifanywe, ili kuvutia watalii wengi zaidi kutoka China kuangalia vivutio mbalimbali vya utalii vya Tanzania, kuanzia mbuga za wanyamapori hadi fukwe za baharini.