Mamlaka nchini Tanzania jana zimetangaza hatua zinazolenga kuimarisha usalama katika Ziwa Victoria, ikiwemo kujenga kituo cha kikanda cha uratibu wa uokoaji wa majini.
Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi wa Tanzania Bw. Makame Mbarawa ameliambia bunge kwamba kituo kicho kitajengwa katika eneo la Ilemela, mkoani Mwanza, chini ya uratibu wa Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC). Amesema mipango inaendelea ya kujenga vituo vingine vitatu vya utafutaji na uokoaji kwenye maeneo ya Kanyala mkoani Geita, Nansio-Ukerewe mkoani Mwanza, na Musoma mkoani Mara, ambayo yote yako kando ya Ziwa hilo.
Amesema TASAC imetoa zabuni ya kimataifa kwa ajili ya utengenezaji wa boti moja ya matibabu na mbili za utafutaji na uokoaji, na kuongeza kuwa, kwa kushirikiana na Mamlaka ya Hali ya Hewa ya Tanzania, Shirika hilo linatoa utabiri wa hali ya hewa mara kwa mara kuhusu Ziwa Victoria ili kuhakikisha usalama wa watumiaji wa ziwa hilo.