Kenya yarejea ahadi yake ya ulinzi wa viumbehai licha ya kuongezeka kwa matishio
2023-05-23 08:23:01| CRI

Kenya imeadhimisha Siku ya Kimataifa ya Anuai ya Viumbehai jana jumatatu kwa maofisa wa ngazi ya juu wakirejea ahadi zao za kulinda spishi ambazo kwa sasa zinakabiliwa na matishio mbalimbali.

Waziri wa Mazingira, Mabadiliko ya Tabianchi na Misitu, Soipan Tuya amesema, upotevu wa anuai ya viumbehai nchini humo inaleta wasiwasi, hivyo kuna umuhimu wa kuharakisha hatua endelevu za uhifadhi. Amesema mazingira ya asili yanapungua nchini Kenya kwa kiwango ambacho hakijatarajiwa katika historia ya binadamu, na kiwango cha kutoweka kwa spishi mbalimbali kinaongezeka na kuleta athari kubwa kwa watu.

Amesema nchi hiyo imeandaa mipango ya kusitisha na kurejesha anuai ya viumbe kama ilivyoelekezwa kwenye Mpango wa Kimataifa wa Kunming-Montreal wa Anuai ya Viumbe ambao ulifikiwa mwaka 2022, unaolenga kuongeza ulinzi wa spishi zilizo hatarini.