Kampuni ya kutengeneza mabasi ya China, Yutong, jana jumanne imezindua mabasi ya kwanza ya umeme ya usafiri wa umma mjini Lagos, Nigeria, wakati nchi hiyo ikijiandaa kuachana na mabasi yanayotumia mafuta na kutumia magari ya umeme.
Mradi huo ni uratibu wa pamoja kati ya kampuni ya Oando Clean Energy, ambayo ni mwenza wa kampuni ya Yutong nchini Nigeria, na Mamlaka ya Uchukuzi ya mji wa Lagos, na umeanza kwa mabasi mawili ya umeme ya Yutong katika barabara ya mabasi ya mwendokasi mjini Lagos.
Akizungumza katika uzinduzi wa mradi huo, gavana wa Lagos Babajide Sanwo-Olu amesema, hatua hiyo inaendana na malengo ya mji huo kuwa mji wa kisasa. Pia amesema, mfumo wa usafiri wa umma nchini Nigeria unataka kuchukua nafasi chanya katika kupunguza utoaji wa hewa chafu, na kuongeza kuwa mabasi mapya ya umeme yatapunguza utoaji wa hewa chafu na pia kuongeza ufanisi.