Jiji la New York linadidimia kutokana na mamilioni ya majengo yake mazito.
2023-05-24 23:27:38| cri

Utafiti mpya uliofanyika nchini Marekani unaonyesha kuwa Jiji la New York linadidimia kutokana na uzito wa jumla wa majengo yake.

Mchakato wa kudidimia taratibu umetajwa kuwa unaweza kuleta matatizo kwa jiji hilo ambalo kina cha bahari kimekuwa kikipanda zaidi ya mara mbili ya kiwango cha kimataifa, na kinatarajiwa kupanda kati ya inchi 8 na inchi 30 ifikapo 2050.

Mwandishi mkuu wa utafiti huo Bw Tom Parsons, ambaye ni mtaalamu wa jiofizikia katika Utafiti wa Jiolojia wa Marekani, amesema mbali na uzito wa majengo kuna matukio mengine yanayosababisha hali hiyo, lakini kumekuwa na matukio kadhaa makubwa ya kimbunga kama Sandy na Ida huko New York, ambapo mvua kubwa ilisababisha mafuriko katika jiji hilo, na baadhi ya athari za ukuaji wa miji zimeruhusu maji kuingia.

Utafiti huo umechapishwa kwenye jarida la Earth’s Future, ukienda kuonyesha jinsi majengo marefu katika maeneo ya pwani, kando ya mito au kando ya maziwa yanavyoweza kuchangia hatari ya mafuriko katika siku zijazo, na kwamba hatua zinapaswa kuchukuliwa ili kupunguza athari zinazoweza kusababisha hatari.