Mapigano ya hapa na pale yametokea kati ya Jeshi la Sudan na Kikosi cha RSF huko Khartoum, mji mkuu wa Sudan, ingawa pande hizo mbili zimesaini makubaliano ya kusimamisha vita kwa siku saba yaliyoanza kutekelezwa jumatatu wiki hii.
Kwa mujibu wa mashuhuda, mapigano hayo yalitokea katika mji wa Omdurman na maeneo ya kusini mwa Khartoum.
Habari nyingine zinasema, Umoja wa Mataifa na wenzi wake nchini Sudan, jana wameanza kufikisha misaada kwa watu wengi kadiri iwezekanavyo katika sehemu zinazoheshimu makubaliano ya kusimamisha vita.
Ofisi ya Uratibu wa Masuala ya Kibinadamu ya Umoja wa Mataifa (OCHA) imesema, malori 20 yaliyobeba vifaa kutoka Shirika la Kuhudumia Watoto la Umoja wa Mataifa na Shirika la Kimataifa la Uhamiaji yamepelekwa katika sehemu tofauti za nchini Sudan.