Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amepongeza kukamatwa kwa Fulgence Kayishema nchini Afrika Kusini, mmoja wa washukiwa waliosakwa wa mauaji ya kimbari ya mwaka 1994 dhidi ya Watutsi nchini Rwanda.
Kwa mujibu wa Mahakama ya kimataifa ya kesi za jinai zilizobaki (International Residual Mechanism for Criminal Tribunals), Kayishema aliyezuiliwa mwaka 2001, alikamatwa Jumatano alasiri mjini Paarl, Afrika Kusini katika operesheni ya pamoja.
Bw. Guterres amepongeza ushirikiano kati ya shirika hilo na mamlaka za Afrika Kusini kwa kumkamata Bw. Kayishema.
Mwaka 2001 Kayishema alishtakiwa na iliyokuwa Mahakama ya Kimataifa ya Mauaji ya Kimbari ya Rwanda kwa tuhuma nyingi za mauaji ya halaiki, na uhalifu mwingine uliofanywa katika Wilaya ya Kivumu, Mkoa wa Kibuye.