Rais wa Uganda asaini mswada wa kupambana na ushoga kuwa sheria
2023-05-30 08:41:56| CRI

Spika wa bunge la Uganda Bibi Anita Among amesema Rais Yoweri Museveni amesaini mswada wa kupambana na ushoga kuwa sheria, na kuweka adhabu ya kifo na kifungo cha maisha gerezani kwa baadhi ya vitendo vya mapenzi ya jinsia moja, na kifungo cha hadi miaka 20 gerezani kwa kuendeleza na kufadhili shughuli za mapenzi ya jinsia moja.

Jumla ya wabunge 371 waliupigia kura mswada wa sheria hiyo baada ya Rais Museveni kuurudisha bungeni kwa ajili ya kuangaliwa upya na kufanyiwa marekebisho mwezi Mei. Bibi Among amesema sasa ni wajibu wa watekeleza sheria kuitekeleza sheria hiyo kwa njia ya haki, thabiti na madhubuti.

Mswada wa kupambana na ushoga nchini Uganda ulitungwa mwaka 2014 na kukosolewa vikali kimataifa, na baadaye ulibatilishwa na Mahakama ya Katiba ya nchi hiyo, kwa kuwa ulipitishwa bila kuwa na idadi ya lazima ya wabunge.