Mkuu wa jeshi la Sudan atishia kutumia "nguvu kamili" dhidi ya kundi la RSF
2023-05-31 08:40:16| CRI

Mkuu wa jeshi la Sudan Jenerali Abdel Fattah Al- Burhan ameonya kuwa jeshi la Sudan litatumia "nguvu kamili" dhidi ya wapiganaji wa Kikosi cha Msaada wa Haraka (RSF) kama kikosi hicho hakitatumia busara.

Akiongea wakati ukaguzi wa baadhi ya vikosi vya jeshi la Sudan, Jenerali Al-Burhan amesema jeshi la Sudan linapigana kwa niaba ya watu na bado halijatumia nguvu zake zote, na kuongeza kuwa jeshi litalazimika kufanya hivyo kama kikosi cha RSF haitatii au kuitikia mwito wa busara.

Amesema vikosi vyote vya jeshi viko kwenye maeneo yote yaliyotawaliwa baada ya kuchukua udhibiti wa maeneo yote ya nchi, na vitaendelea kuwa tayari kupambana hadi ushindi.

Wakati huo huo Jenerali Al-Burhan amethibitisha kuwa jeshi la Sudan limekubali kurefusha makubaliano ya kusitisha mapigano, ili kurahisisha ufikiaji wa huduma kwa raia.

Jumatatu Saudi Arabia na Marekani zilitangaza kwenye taarifa ya pamoja kuwa pande zinazozozana za Sudan zimekubali kurefusha makubaliano ya kusitisha mapigano kwa siku tano zaidi.