Umoja wa Afrika wasema hakuna suluhu la kijeshi kwenye mgogoro wa Sudan
2023-05-31 08:40:45| CRI

Umoja wa Afrika umelaani vikali mgogoro unaoendelea kati ya jeshi la Sudan na Vikosi vya Msaada wa Haraka (RSF) ambao umesababisha mauaji ya raia wasio na hatia, uharibifu mkubwa wa miundombinu, na kusema mgogoro huo hauna suluhu ya kijeshi.

Taarifa iliyotolewa na Umoja huo imesema mgogoro huo umesababisha hali mbaya ya kibinadamu na ukiukwaji mkubwa wa Sheria ya Kimataifa ya Kibinadamu na Sheria ya Kimataifa ya Haki za Kibinadamu.

Umoja wa Afrika umesisitiza kuanzishwa tena kwa mchakato wa mpito wa kisiasa utakaohitimishwa kwa uchaguzi utakaoleta serikali ya kidemokrasia inayoongozwa na raia. Taarifa hiyo pia imepinga kithabiti aina zote za uingiliaji wa nje nchini Sudan.

Taarifa hiyo imekuja wakati Mwenyekiti wa Kamisheni ya AU Bw. Moussa Faki Mahamat anapanga kuitisha mkutano wa ngazi ya juu wa Umoja wa Afrika kuhusu utatuzi wa mgogoro huo.