Waziri wa Nishati wa Tanzania Bw. January Makamba amesema Tanzania itakomesha kukatika kwa umeme mara kwa mara katika maeneo mengi ya nchi katika muda wa miaka miwili hadi mitatu ijayo, baada ya kukamilika kwa mitambo kadhaa ya kuzalisha umeme inayoendelea kujengwa.
Akiongea bungeni mjini Dodoma Bw. Makamba amesema kituo cha kuzalisha umeme kwa kutumia maji cha Julius Nyerere chenye uwezo wa kuzalisha MW 2,115 kinaendelea kujengwa, ujenzi wake ukiwa umefikia asilimia 87.
Pia amesema mtambo wa kuzalisha umeme kwa nishati ya jua unatarajiwa kuanza mkoani Shinyanga, na pia mipango iko katika hatua za mwisho za kutekeleza miradi ya kuzalisha umeme kwa nishati ya upepo katika mikoa ya Singida na Kilimanjaro, na miradi yote iliyopangwa ya kuzalisha umeme itaunganishwa kwenye gridi ya Taifa.