Mkutano wa pili wa kimataifa wa maparachichi ya Afrika umefanyika mjini Nairobi, ambako maofisa waandamizi, wadau na wakulima wa maparachichi wanaeleza matumaini yao ya kuongeza uuzaji wa maparachichi kwa China.
Katibu mkuu wa idara ya maendeleo ya mazao katika wizara ya kilimo ya Kenya Bw. Phillip Kello Harsama amesema kuongeza uuzaji wa maparachichi kwa China, kutakuwa muhimu katika kuongeza mapato ya fedha za kigeni kwa Kenya.
Amesema watawahamasisha wakulima wengi wa Kenya kupanda maparachichi aina ya Hass yanayoagizwa na China.
Mkurugenzi mkuu wa mamlaka ya usimamizi wa afya ya mimea ya Kenya Bw. Theophilus Mutui, amesema serikali ya Kenya imetoa kipaumbele kwa utekelezaji wa hatua za karantini ili kuhimiza uuzaji wa maparachichi kwenye masoko mapya ikiwa ni pamoja na China.