China yapinga kauli ya Blinken juu ya “kuondoa hatari”
2023-06-02 09:00:03| CRI

Msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya China Bi. Mao Ning Alhamisi alipinga kauli ya waziri wa mambo ya nje wa Marekani Antony Blinken juu ya “kuondoa hatari”.

Kwa mujibu wa vyombo vya habari, tarehe 31 Mei Blinken alipozungumza na wanahabari baada ya mkutano wa ngazi ya mawaziri wa baraza la biashara na teknolojia la Marekani na Umoja wa Ulaya alisema, kuhusiana na China, Marekani na Umoja wa Ulaya hazitaki makabiliano, vita baridi au utengano, bali zinafuatilia kuondoa hatari.

Juu ya kauli hiyo, Mao Ning alisema kabla ya kutaja kuondoa hatari, inapaswa kuelewa hatari ni nini. China inadhamiria kithabiti kuzidi kufungua milango yake kwa kiwango cha juu, na kuziwekea kampuni za nchi zote mazingira ya kibiashara ya kuongeza hadhi ya soko, kufuata utawala wa sheria na kanuni za kimataifa. China inashikilia kushirikiana na nchi nyingine kwenye sekta za biashara, sayansi na teknolojia na uwekezaji chini ya msingi wa kuheshimiana na kunufaishana. China inalinda kithabiti usawa na haki ya kimataifa, na kuhimiza kutatua tofauti kwa njia ya mazungumzo. Nchi kama hii ni chanzo cha fursa, na si hatari.