Mkutano wa 21 wa Wakuu wa Nchi na Serikali za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) uliofanyika Jumatano mjini Bujumbura nchini Burundi, uliidhinisha kuongezewa muda wa miezi sita kuanzia Machi 8, 2023 hadi Septemba 8, 2023, kwa jeshi la kanda ya Afrika Mashariki ili kuimarisha mafanikio mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo. .
Kwa mujibu wa taarifa iliyosomwa na Katibu mkuu wa EAC Peter Mathuki, viongozi wa EAC waliidhinisha kwanza kutumwa kwa kikosi kipya cha kikanda Juni 20, 2022, lakini hadi Novemba 2022 ndio takriban wanajeshi 1,000 wa Kenya walikuwa kikosi cha kwanza cha wanajeshi kati ya vinne vilivyoahidiwa kufika Goma, mji mkuu wa jimbo la Kivu Kaskazini.
Taarifa hiyo ilisema wakuu wa nchi za EAC wamelipongeza jeshi la kanda ya Afrika Mashariki kwa mafanikio yake katika kurejesha amani na usalama mashariki mwa DRC. Aidha wakuu wa nchi walilaani vikali ukiukaji wa usitishaji mapigano mashariki mwa DRC na kuagiza jeshi la kanda ya Afrika Mashariki kuchukua hatua za kukomesha hali hiyo kujirudia.