Sudan yaongeza muda wa kufunga anga yake mpaka Juni 15
2023-06-03 20:09:17| cri

Mamlaka ya Usafiri wa Anga nchini Sudan imeongeza muda wa kufunga anga ya nchi hiyo mpaka Juni 15 mwaka huu, wakati mapigano yakiendelea kati ya Jeshi la Sudan na kikosi cha RSF.

Katika tangazo kwa watoaji wa huduma za usafiri wa anga, mamlaka hiyo imeamua kuongeza muda wa kufungwa kwa anga ya nchi hiyo kwa ndege zote za kiraia, isipokuwa zile zinazopeleka misaada ya kibinadamu, na kuongeza kuwa huenda muda huo ukaongezwa tena katika siku za baadaye.

Tangu mapigano yatokee katika mji mkuu wa Sudan, Khartoum na maeneo mengine April 15, anga ya nchi hiyo imefungwa kutokana na mfumo wa kuongoza ndege katika Uwanja wa Kimataifa wa Khartoum kuathiriwa na mapigano hayo.