Mradi Bwawa la Kidunda nchini Tanzania kugharimu Sh. bilioni 335
2023-06-04 21:10:03| cri

Serikali ya Tanzania imeanza kutekeleza mradi wa Bwawa la Kidunda mkoani Morogoro litakalogharimu Sh bilioni 335, ambalo litakuwa na uwezo wa kuhifadhi maji yatakayotumika kwa miaka mitatu mfululizo.

Hayo yamesemwa na Kaimu Ofisa Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Maji Safi na Maji Taka jijini Dar es Salaam, (DAWASA), Kiula Kingu, wakati akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa mradi huo kwa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya ya Morogoro. Amesema lengo la utekelezaji mradi huo ni kuwezesha mitambo ya maji ya Ruvu Juu na Ruvu Chini kuwa na maji ya kutosha ili kuzalisha maji kipindi cha kiangazi.

Aidha, Kingu amesema Bwawa hilo litakapokamilika, litakuwa na uwezo wa kuhifadhi maji kipindi cha masika ili yaweze kutumika nyakati za kiangazi.