Mkutano wa Baraza la Ushirikiano na Vyombo vya Habari vya ASEAN wa 2023 wafanyika Guangxi, China
2023-06-06 21:21:57| CRI

Mkutano wa Baraza la Ushirikiano na Vyombo vya Habari vya ASEAN wa mwaka 2023, ambao uliandaliwa kwa pamoja na Shirika Kuu la Utangazaji la China CMG na Mkoa wa Guangxi umefanyika Jumanne huko Nanning, mkoani Guangxi, China. Wawakilishi zaidi ya 200 wa vyombo vya habari na mashirika ya kimataifa, pamoja na wataalamu na wasomi kutoka China na nchi za ASEAN wamebadilishana maoni kuhusu mada ya “Uvumbuzi, Ushirikiano na Mustakabali” kwa njia ya mtandao na nje ya mtandao, ili kutoa mchango kwa ajili ya Jumuiya ya China na ASEAN yenye Mustakabali wa Pamoja.

Mkuu wa CMG Shen Haixiong akihutubia baraza hilo ameeleza kuwa, rais Xi Jinping amesifu sana ushirikiano kati ya China na ASEAN, na kuwa na matarajio makubwa juu ya ujenzi wa Jumuiya ya Mustakabali wa Pamoja kati ya pande hizo mbili zenye uhusiano wa karibu zaidi. Utekelezaji wa mpango huo utategemea juhudi za vyombo vya habari, na CMG ikiwa jukwaa kubwa zaidi la kimataifa la vyombo vya habari nchini China, imefanya mawasiliano ya karibu na vyombo vya habari vya nchi za ASEAN na kupata matokeo mazuri. Hadi sasa imetengeneza vipindi kumi vya televisheni na vyombo muhimu vya habari vya nchi sita za ASEAN zikiwa ni pamoja na Laos, Cambodia, Thailand, Myanmar, Indonesia na Malaysia, ili kuonesha hali halisi ya China na ASEAN kwa watazamaji duniani.