Guterres atoa wito wa kuchukuliwa hatua za kimataifa kupunguza uchafuzi wa plastiki
2023-06-06 08:45:52| CRI

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres Jumatatu alitoa wito wa kuchukuliwa hatua za kimataifa ili kupunguza uchafuzi wa plastiki.

Akitoa wito huo kwa njia ya video katika makao makuu ya Umoja wa Mataifa mjini New York kwa ajili ya kuadhimisha Siku ya Mazingira Duniani, inayoangukia Juni 5, na ambayo mwaka huu kaulimbiu yake ni "Ufumbuzi wa Uchafuzi wa Plastiki,  Bw. Guterres alisema kila mwaka, zaidi ya tani milioni 400 za plastiki huzalishwa duniani kote, na theluthi moja hutumiwa mara moja tu. Ameongeza kuwa kila siku, zaidi ya malori 2,000 ya takataka zilizojaa plastiki hutupwa kwenye bahari, mito na maziwa.

Hata hivyo amesema kuna ufumbuzi, mwaka jana, jumuiya ya kimataifa ilianza mazungumzo ya makubaliano ya kisheria ya kukomesha uchafuzi wa plastiki, ambayo ni hatua ya kwanza inayotia matumaini. Ripoti mpya ya Mpango wa Mazingira wa Umoja wa Mataifa inaonesha kuwa, kama tutachukua hatua sasa ya kutumia tena, kuchakata, kubadilisha mwelekeo na kutumia njia mbadala, inawezekana kupunguza uchafuzi wa plastiki kwa asilimia 80 ifikapo mwaka 2040.