China yasisitiza kuwa uingiliaji wa nje na vikwazo vya upande mmoja haviwezi kutatua matatizo yanayoikabili katikati ya Afrika
2023-06-06 08:43:10| CRI

Naibu mwakilishi wa kudumu wa China katika Umoja wa Mataifa Balozi Dai Bing amesisitiza kuwa uingiliaji wa nje na vikwazo vya upande mmoja haviwezi kutatua matatizo yanayozikabili nchi za katikati ya Afrika.

Balozi Dai amesema hayo alipohutubia Mkutano wa wazi wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuhusu suala la eneo la katikati ya Afrika, na kuongeza kuwa China inaona kuwa jumuiya ya kimataifa inatakiwa kutathmini kazi ya haki za binadamu kutokana na hali halisi ya nchi na mahitaji ya wananchi, na haipaswi kuchukulia haki za binadamu kama kauli mbiu tupu, haswa kuwa chombo cha kuingilia kati mambo ya ndani ya nchi nyingine.

Amesisitiza kuwa China inaunga mkono Jumuiya ya Uchumi ya Nchi za Katikati ya Afrika kufuata wazo la pamoja la usalama, na kuimarisha ushirikiano wa usalama wa pamoja. Pia amesema China ni rafiki na mwenzi mzuri wa nchi za katikati ya Afrika, na inaunga mkono kithabiti maendeleo ya amani ya kanda hiyo, na kwamba China inapenda kushirikiana na jamii ya kimataifa kuongeza ufuatiliaji na fedha katika kanda hiyo, ili kutoa misaada mingi zaidi ya kiujenzi.