China na Afrika Kusini zaahidi kuimarisha ushirikiano wa kimkakati wa kina
2023-06-07 09:24:12| CRI

Waziri wa Mambo ya Nje wa China Qin Gang Jumanne alizungumza kwa simu na Waziri wa Uhusiano wa Kimataifa na Ushirikiano wa Afrika Kusini Naledi Pandor, wakati ambapo pande hizo mbili ziliapa kuzidisha ushirikiano wa kina wa kimkakati kati ya nchi hizo mbili.

Katika mazungumzo yao, Bw. Qin alisema ushirikiano wa kivitendo kati ya China na Afrika Kusini katika nyanja mbalimbali umekuwa na matokeo mazuri katika miaka ya hivi karibuni. Vilevile alisema Rais Xi Jinping wa China na mwenzake wa Afrika Kusini, Cyril Ramaphosa, walikutana mwezi Novemba mwaka jana kando ya Mkutano wa Kilele wa Kundi la nchi 20 wa Bali, ambapo pande hizo mbili zilifikia makubaliano muhimu juu ya kukuza zaidi maendeleo ya uhusiano kati ya nchi hizo mbili.

Kwa upande wake, Pandor alisema Afrika Kusini inatilia maanani sana kuendeleza uhusiano wake na China, na inazingatia kwa dhati sera ya China moja. Afrika Kusini iko tayari kuungana na China kuzidisha ushirikiano wa kivitendo katika nyanja mbalimbali, ili kuufikisha ushirikiano wa kimkakati wa kina kati ya China na Afrika Kusini katika ngazi mpya.