Kenya Jumatano ilizindua mfuko wa shilingi milioni 330 (sawa na dola milioni 2.37 za kimarekani) ili kuboresha upatikanaji wa maji safi nchini humo.
Katika hotuba ya Waziri wa Maji, Usafi wa Mazingira na Umwagiliaji, Alice Wahome, iliyosomwa kwa niaba yake na Mkurugenzi wa Usimamizi wa Usafi wa Mazingira na Mkuu wa Ushirikiano wa Maendeleo katika wizara hiyo Kimathi Kyengo, mbele ya ya wanahabari mjini Naiŕobi, Kenya, alisema fedha hizo zitatolewa kwa watoa huduma wadogo wa maji bila kuhitaji dhamana, na kwamba mfuko huo unatarajiwa kufadhili miradi ambayo itatoa huduma ya maji kwa takriban watu 200,000 kote nchini Kenya. Kyengo alibainisha kuwa mfuko huo utaongeza uwezo wa kutoa mikopo kwa watoa huduma za maji mijini na vijijini.
Naye Kaimu Mkurugenzi wa Leseni, Viwango na Utetezi wa Bodi ya Udhibiti wa Huduma za Maji, Angela Kimani, alisema kwa sasa asilimia 70 ya wananchi wanapata maji safi nchini humo.