Tume ya Mpito ya Umoja wa Afrika nchini Somalia (ATMIS) na Umoja wa Mataifa wamelaani shambulizi la kigaidi dhidi ya hoteli moja lililotokea Ijumaa iliyopita mjini Mogadishu, Somalia ambapo watu tisa waliuawa na wengine kumi kujeruhiwa.
Mashirika hayo yamesema kuwa mashambulizi ya kigaidi likiwemo shambulizi hilo dhidi ya hoteli ya Pearl Beach yaliyofanywa na kundi la al-Shabab hayatazuia juhudi za kuleta utulivu nchini Somalia. Polisi wa Somalia Jumamosi iliyopita walisema kuwa jeshi la usalama lilizingira hoteli hiyo kwa saa saba na kufanikiwa kuwaua wapiganji wote saba wa kundi la al-Shabab walioshiriki kwenye shambulizi hilo na watu 84 walionaswa hotelini wameokolewa kwa usalama.