Takriban watuhumiwa 16 wanashikiliwa na Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya nchini Tanzania (DCEA) wakihusishwa na kilimo cha hekta 953 za bangi.
Kwenye taarifa yake iliyotoa jana Jumapili DCEA ilisema watuhumiwa hao walikamatwa wakati wa msako mkali wa siku nane kwa watu wanaoendesha kilimo cha bangi mkoani Arusha ulioanza Mei 31. Taarifa hiyo ilifafanua kuwa wakati wa operesheni iliyofanywa mahususi kwenye maeneo ya chini ya Mlima Meru, hekta 953 za bangi ziliharibiwa na mamlaka hiyo wakishirikiana na polisi.
Kamishna Mkuu wa DCEA Aretas Lyimo amesema msako huo ulikuwa na nia ya kudhibiti kilimo cha bangi nchini Tanzania na utakuwa endelevu. Kwa mujibu wa sheria ya Udhibiti na Utekelezaji wa Dawa za Kulevya ya mwaka 2015, ni kinyume cha sheria kumiliki au kutumia bangi nchini Tanzania.