Marais wa China na Honduras waweka dira kwa uhusiano wa nchi mbili kwenye mkutano wa kihistoria
2023-06-13 09:20:57| CRI

Rais Xi Jinping wa China jana Jumatatu alifanya mazungumzo na mwenzake wa Honduras Bibi Iris Xiamara Castro Sarmiento ambaye yuko ziarani hapa Beijing, akiahidi kushirikiana pamoja na upande wa Honduras kuelekeza uhusiano wa nchi hizo mbili upige hatua kubwa zaidi kwa mtazamo wa kimkakati na wa muda mrefu, na kubadilisha ruwaza yao ya ushirikiano kuwa matokeo halisi kwa ajili ya maslahi ya watu wa pande hizo mbili.

Rais Xi ameitaja ziara ya Rais Xiamara Castro ambaye ni rais wa kwanza wa Honduras kufanya ziara nchini China, kuwa “imefungua ukurasa mpya kwenye historia ya uhusiano kati ya China na Hondura”.

Rais Xi amesema uhusiano wa nchi hizo mbili umekuwa na mwanzo mwema wenye msukumo mkubwa na mustakbali mzuri tangu China na Honduras zianzishe uhusiano wa kibalozi mwezi Machi mwaka huu.

Kwa mujibu wa taarifa ya pamoja iliyotolewa baada ya mazungumzo yao kumalizika, China na Honduras zimekubaliana kuimarisha mwongozo wa kisiasa, kuhimiza mawasiliano kwenye ngazi zote, na kuendeleza mawasiliano ya kiutamaduni na ushirikiano katika nyanja zote, na nchi hizo mbili zitakuwa marafiki na wenzi wazuri wanaoheshimiana na kunufaishana, wenye usawa na maendeleo ya pamoja.