Ubalozi wa China nchini Zimbabwe ulifanya hafla ya uchangiaji Jumanne mjini Harare, Zimbabwe, ili kuleta furaha kwa mayatima na watoto wengine wanaoishi katika mazingira magumu nchini humo.
Watoto kutoka kituo cha mayatima cha Hupenyu Hutsva cha Harare walipokea vifurushi vikiwa vimesheheni mablanketi, mboga na vifaa vya kuandikia. Msaada huo ni sehemu ya kampeni ya huduma ya afya kwa watoto wa Afrika iliyopewa jina la "Kufurahisha Mioyo ya Watoto: Hatua ya Pamoja ya China na Afrika," ambayo ilianzishwa kwa pamoja na mke wa Rais wa China Peng Liyuan, na Shirika la Wake wa Marais wa Afrika kwa Maendeleo. Timu ya madaktari wa China nchini Zimbabwe pia iliwafanyia uchunguzi wa kimatibabu bila malipo watoto wapatao 100 baada ya sherehe hiyo.
Katika hotuba iliyosomwa kwa niaba yake na Naibu Waziri wa Serikali za Mitaa na Kazi za Umma Marian Chombo, Mke wa Rais wa Zimbabwe Auxillia Mnangagwa alitoa shukrani kwa Peng kwa mchango huo.
Naye Balozi wa China nchini Zimbabwe Zhou Ding alisema China itaendelea kuunga mkono suala la watoto nchini Zimbabwe ili kuboresha ustawi wa makundi yaliyo katika mazingira magumu nchini humo.