Mji wa Hangzhou nchini China wasema uko tayari kwa ufunguzi wa Michezo ya Asia
2023-06-14 21:23:20| cri

Mji wa Hangzhou nchini China uko tayari kuandaa Michezo ya 19 ya Asia kwa kuzingatia kanuni za kijani na endelevu zinazoungwa mkono na teknolojia ya hali ya juu, waandaaji wa michezo hiyo wamesema Jumatano.

"Kama viwanja vilivyopo vinaweza kukarabatiwa ili kufikia viwango vya Michezo ya Asia, hakuna haja ya kujenga vipya, kwa hivyo ni viwanja 12 tu kati ya 56 vya mashindano ya Michezo ya Asia ya Hangzhou ndivyo vimejengwa upya," Meya wa Mji wa Hangzhou Yao Gaoyuan ameuambia mkutano na waandishi wa habari uliofanyika Beijing.

Nishati ya kijani, kama vile nishati ya jua na upepo, imetumika kwa wingi katika maeneo yote ya Michezo. Zaidi ya hayo, huduma za mtandaoni, bidhaa za kidijitali, na vifaa vinavyotumia teknolojia ya hali ya juu viko tayari, vikitazamia kwa hamu kuwasili kwa washiriki kutoka kote Asia ndani ya takriban siku 100.

Zhou Jinqiang, Naibu Mkuu wa Kamati ya Maandalizi ya Michezo ya Asia ya Hangzhou (HAGOC), amethibitisha katika mkutano huo na waandishi wa habari kwamba Kamati zote 45 za Olimpiki za kitaifa na kikanda barani Asia zimejiandikisha kwa ajili ya Michezo ya Asia ya Hangzhou, hali inayoonyesha "shauku kubwa" kwa michezo hiyo.

Ameongeza kuwa zaidi ya wanamichezo 900 wa China watashiriki kwenye michezo hiyo.

Kwa mujibu wa HAGOC, zaidi ya watu milioni 8 tayari wametembelea viwanja vya mashindano na mazoezi.

Li Yanyi, Naibu Gavana wa Mkoa wa Zhejiang, amesema katika mkutano na waandishi wa habari kwamba kuandaa Michezo ya Asia kumechangia katika uboreshaji wa mifumo ya usafiri katika Mji wa Hangzhou na miji mingine mwenyeji, ikiwa ni pamoja na Ningbo, Wenzhou, Huzhou, Shaoxing na Jinhua.

Amesema, hivi sasa, Hangzhou imekamilisha ujenzi wa reli yenye urefu wa kilomita 516 na mtandao wa barabara kuu wenye urefu wa kilomita 480, kuhakikisha usafirishaji mzuri wakati wa michezo hiyo na kuanzisha msingi imara wa maendeleo jumuishi ya muda mrefu ya Delta ya Mto Yangtze.

“Ili kuadhimisha kusalia siku 100 kuelekea Michezo ya Asia ya Hangzhou leo Alhamisi, moto wa Asia utawashwa katika magofu ya kiakiolojia ya mji wa kale wa Liangzhu huko Zhejiang na miundo ya medali itatolewa,” Li amesema.