Ethiopia yatoa mafunzo kwa watoa huduma ya kwanza kukabiliana na dharura za afya ya umma
2023-06-14 08:46:02| CRI

Ethiopia imetoa mafunzo kwa timu ya watoa huduma ya kwanza 100 ili katika siku zijazo waweze kukabiliana na dharura za afya ya umma na majanga ya kibinadamu nchini Ethiopia na kwingineko.

Watoa huduma hao walipewa mafunzo na Shirika la Afya Duniani (WHO) kwa ushirikiano na Wizara ya Afya ya Ethiopia, Taasisi ya Afya ya Umma ya Ethiopia, na Kituo cha Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa Afrika (Africa CDC).

Kwa mujibu wa taarifa ya WHO, mafunzo hayo yanalenga kuhakikisha kuwa kila nchi ya Afrika inajiandaa kukabiliana na dharura za kiafya na majanga ya kibinadamu ndani ya saa 24 hadi 48 tangu tukio linapotokea.

Taarifa hiyo ilimnukuu Waziri wa Afya wa Ethiopia Dereje Duguma akisema, Ethiopia inakabiliwa na dharura za kiafya na inahitaji uratibu thabiti na mafunzo sahihi ili kujiandaa, kuzuia, na kuitikia mara moja iwapo kutatokea mlipuko wa magonjwa.