Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan amewapiga marufuku wakulima nchini humo kuuza mazao yao nje ya nchi ili kukabiliana na upungufu wa chakula nchini humo.
Akizungumza jana jumanne jijini Mwanza alipokuwa mgeni rasmi kwenye Tamasha la Utamaduni la Bulabo linaloendelea katika Uwanja wa Red Cross Ngomeni Kisesa jijini humo, rais Samia amesema ametoa maagizo kwa Wizara za Fedha na Wizara ya Kilimo nchini humo kuhakikisha wananunua mazao kutoka kwa wakulima msimu huu wa mavuno ili nchi iwe na akiba ya chakula cha kutosha.
Amesema kwa sasa Tanzania ina akiba ya chakula tani laki mbili hadi laki mbili na nusu, na serikali yake inapanga kununua chakula zaidi ili kuwa na hifadhi ya chakula tani laki tano kwa mwaka huu.