Vijana 99 kati ya 100 wa Tanzania waliokuwa wanapatiwa mafunzo ya kilimo cha kisasa kwa njia ya vitendo katika Kituo cha Kimataifa cha Mafunzo ya Kilimo cha Arava kilichopo kusini mwa Israel, wamehitimu mafunzo na kutunukiwa vyeti katika mahafali yaliyofanyika jumatatu wiki hii.
Katika hotuba yake, Balozi wa Tanzania nchini Israel, Alex Kallua aliwapongeza wahitimu wote na kuwaasa kuwa chachu ya mabadiliko wanaporejea nchini kwao kwa kufanyia kazi kwa vitendo mafunzo waliyoyapata nchini Israel.
Katika mahafali hayo, mradi mmoja kutoka kwa vijana wa Tanzania ulishinda tuzo ya Dola za Marekani 6,000 kutoka kwa The Dean Family Fellowship Grant, kufuatia shindano la kuandika na kuwasilisha mradi ambao vijana husika watafanya na kuleta mabadiliko chanya kwao na kwa jamii inayowazunguka, mara baada ya kurejea katika nchi zao.