Rais Xi Jinping wa China jana Jumatano alitoa pendekezo lenye vipengele vitatu kuhusu utatuzi wa suala la Palestina alipofanya mazungumzo na mwenzake wa Palestina Mahmoud Abbas ambaye yuko ziarani hapa Beijing.
Rais Xi amesisitiza kuwa suala la Palestina limekuwa halijatatuliwa katika nusu karne iliyopita na kuleta machungu makubwa kwa watu wa Palestina, na kwamba haki lazima itendeke kwa Palestina haraka iwezekanavyo.
Pendekezo la Rais Xi lina vipengele vitatu vifuatavyo: Kwanza, suluhu ya kimsingi iko katika uanzishwaji wa nchi huru ya Palestina yenye mamlaka kamili kwenye msingi wa mipaka iliyoamuliwa mwaka 1967, Jerusalem ikiwa ni mji mkuu wake; Pili, mahitaji ya kiuchumi ya Palestina yanahitaji kufikiwa, na jumuiya ya kimataifa inahitaji kuongeza msaada wa kimaendeleo na kibinadamu kwa Palestina; Tatu, ni muhimu kudumisha mwelekeo sahihi wa mazungumzo ya amani.
Rais Xi amesema, China iko tayari kubeba jukumu muhimu katika kuisaidia Palesina kutimiza maafikiano ya ndani na kuhimiza mazungumzo ya amani.