Chuo cha Diplomasia cha Venancio de Moura (ADVM) nchini Angola Jumatano kilisaini makubaliano ya maelewano na Taasisi ya Confucius ya Chuo Kikuu cha Agostinho Neto (UAN) kwa ajili ya kuanzisha darasa litakalofundisha lugha ya Kichina na utamaduni katika Chuo hicho cha diplomasia.
Venancio de Moura kitakuwa chuo kikuu cha pili cha Angola baada ya chuo cha Agostinho Neto kutoa rasmi kozi za lugha ya Kichina kwa msaada wa Taasisi ya Confucius nchini humo.
Mkurugenzi mkuu wa ADVM, Jose Marcos Barrica, katika hotuba yake alielezea umuhimu wa makubaliano hayo, akisema kuwa darasa litakuwa na jukumu muhimu katika kuimarisha uhusiano kati ya watu wa Angola na China. Akisisitiza faida za muda mrefu kutokana na kufunguliwa kwa darasa hilo, Pedro Magalhaes, mkuu wa UAN, alisema fursa hii itawawezesha kufikia mafanikio makubwa kwa manufaa ya Angola na China. Akizungumza katika hafla hiyo, Balozi wa China nchini Angola, Gong Tao, alisema darasa hilo litatoa msukumo mpya kwa ushirikiano wa kitamaduni kati ya China na Angola.