Mamlaka ya Maendeleo ya Kiserikali (IGAD) imetoa ripoti ikisema, msukosuko wa chakula utaongezeka katika Afrika Mashariki na pembe ya Afrika mwaka huu.
Ripoti hiyo yenye kichwa cha “Ufuatiliaji wa Kikanda wa IGAD wa Ripoti ya Kimataifa kuhusu Msukosuko wa Chakula 2023 ” imesema, watu wapatao milioni 30 wanakadiriwa kuhitaji msaada wa kibinadamu wa chakula nchini Kenya, Somalia, Sudan Kusini, Sudan na Uganda.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, kati ya watu milioni 30 wanaokabiliwa na uhaba wa chakula, watu milioni 7.5 wa nchini Kenya, Somalia, Sudan Kusini na Sudan watakabiliwa na ukosefu mkubwa wa chakula na kuhitaji hatua za dharura.
Imeongeza kuwa, watu zaidi ya 83,000 wanakabiliwa na ukosefu mkubwa zaidi wa chakula katika maeneo ya kanda hiyo yanayokumbwa na ukame mkali na kuathiriwa na vita, hasa nchini Somalia na Sudan Kusini.