Tunisia yatarajia kuimarisha uhusiano wa biashara na uwekezaji na China
2023-06-16 09:09:19| CRI

Maofisa wa biashara wa Tunisia wamesisitiza mustakbali mkubwa wa kuimarisha uhusiano wa biashara na uwekezaji na China.

Akiongea kwenye mkutano wa uchumi na biashara kati ya Tunisia na China uliofanyika Tunis, makamu wa kwanza wa mwenyekiti wa Shirikisho la Makampuni ya Raia la Tunisia (CONECT International) Salma Elloumi amesema kuwa hili ni jambo linalowezekana na linaloweza kutimizwa kutokana na mustakabali kwenye nyanja za teknolojia ya kijani, nishati endelevu, utengenezaji wa dawa, ujenzi na miundombinu, afya, utalii na uvumbuzi wa kiteknolojia na kidijitali.

Takwimu zilizotolewa kwenye mkutano huo zimeonesha kuwa thamani ya biashara kati ya Tunisia na China imefikia dola za kimarekani milioni 763 katika kipindi cha miezi minne iliyopita kuanzia Januari hadi Aprili mwaka huu, ikiwa ni ongezeko la asilimia 12.5 kuliko mwaka jana muda kama huo.