UM: Idadi ya vifo kutokana na mlipuko wa kipindupindu nchini Ethiopia yafikia 153
2023-06-16 09:08:42| CRI

Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kuratibu Masuala ya Kibinadamu (OCHA) imesema kuwa idadi ya vifo kutokana na mlipuko wa ugonjwa wa kipindupindu unaoendelea nchini Ethiopia imeongezeka hadi 153.

Kwenye ripoti yake mpya iliyotolewa Jumatano, OCHA imesema mlipuko huo wa kipindupindu unaoenea katika wilaya 85 za mikoa ya Oromia, Kusini, Somali na Sidama nchini Ethiopia umewaathiri watu zaidi ya elfu kumi, na kwamba huo ni mlipuko uliodumu kwa muda mrefu zaidi nchini humo, ambao kesi ya kwanza ya maambukizi ilirekodiwa mwezi Agosti mwaka 2022.

Kwa mujibu wa OCHA, ni asilimia 24 tu ya dola bilioni 4 za kimarekani zinazohitajika kutekeleza Mpango wa Mwitikio wa Kibinadamu nchini Ethiopia kwa mwaka huu, ndio zimepatikana mpaka sasa.