FAO yazindua mradi wa kuzuia kuenea kwa viwavijeshi Mashariki mwa Afrika
2023-06-16 08:55:09| CRI

Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO) Alhamisi lilizindua mradi katika mji wa Naivasha nchini Kenya ili kulinda mazao ya chakula kutokana na hasara kubwa inayosababishwa na viwavijeshi, wadudu ambao wanaweza kuharibu hadi asilimia 100 ya vyakula vikuu kama wataachwa bila kudhibitiwa.

Mradi huo, unaojulikana kama Usaidizi wa Dharura wa Kudhibiti Milipuko na Uvamizi wa Viwavijeshi Mashariki mwa Afrika, unalenga kutumia uwezo wa kitaifa katika Mashariki mwa Afrika dhidi ya uvamizi wa wadudu hao.

Mkurugenzi wa Kitengo cha Uzalishaji na Ulinzi wa Mimea katika FAO Xia Jingyuan, alisema wadudu hao ni tishio kubwa la kusababisha uhaba wa chakula katika eneo hilo, na hivyo kulazimisha uingiliaji wa haraka wa FAO na washirika wake ili kuzuia upotezaji mkubwa wa mazao, ambayo tayari yamepungua kutokana na shinikizo la ukame wa muda mrefu.