Waziri Mkuu wa China atoa wito wa maendeleo mapya katika uhusiano kati ya China na Ujerumani
2023-06-19 09:43:23| CRI

Waziri Mkuu wa China Li Qiang Jumapili aliwasili Berlin nchini Ujerumani kwa ziara rasmi, ambapo pia atafanya mashauriano ya saba kati ya serikali za China na Ujerumani.

Bw. Li alisema Beijing iko tayari kushirikiana na Berlin kutafuta uwezekano zaidi wa ushirikiano na kuchochea maendeleo mapya katika uhusiano wa pande mbili. Ujerumani kikiwa ni kituo chake cha kwanza katika ziara yake ya kwanza ya nje ya nchi tangu awe waziri mkuu wa China, Li alibainisha kuwa ziara hii itaendeleza urafiki wa jadi wa nchi hizo mbili na kuimarisha ushirikiano wao.

Li alisema China iko tayari kufanya mazungumzo ya uwazi na ya kina na Ujerumani kwa kuzingatia kanuni za kuheshimiana, kutafuta maelewano huku wakiondoa tofauti, na kunufaishana pande zote mbili, kwa ajili ya kuchunguza zaidi uwezekano wa ushirikiano, kushughulikia tofauti ipasavyo na kuimarisha ushirikiano wao wa kimkakati wa pande zote, ili kutoa ishara chanya na thabiti ya kudumisha minyororo ya usambazaji wa kimataifa na amani na ustawi duniani.