Mawaziri wa mambo ya nje wa China na Marekani wafanya mazungumzo
2023-06-19 09:46:47| CRI

Waziri wa Mambo ya Nje wa China Qin Gang alifanya mazungumzo na mwenzake wa Marekani Antony Blinken jana Jumapili hapa Beijing.

Qin ameeleza kuwa kwa sasa uhusiano kati ya China na Marekani upo katika hatua mbaya zaidi tangu kuanzishwa kwake, hali ambayo hailingani na maslahi ya msingi ya watu wa nchi hizi mbili wala matarajio ya pamoja ya jamii ya kimataifa. Amesema sera ya China kuhusu Marekani bado ni thabiti, na kwamba inaongozwa na kanuni za kuheshimiana, kuishi pamoja kwa amani na ushirikiano wa kunufaisha zilizotolewa na rais Xi Jinping wa China, ambazo pia zinapaswa kuzingatiwa kama moyo unaoshikiliwa pamoja, mstari mwekundu unaolindwa na lengo linalofuatwa na nchi hizo mbili kwa pamoja.

Ameongeza kuwa China imejitahidi kujenga uhusiano tulivu, unaotabirika na wa kiujenzi na Marekani, na China inatumai kuwa Marekani itakuwa na mtazamo sahihi na wenye busara kuhusu uhusiano wake na China, kufanya kazi pamoja na China ili kulinda msingi wa kisiasa wa uhusiano kati ya China na Marekani, na kushughulikia matukio yasiyotarajiwa kwa utulivu, utaalamu na busara.

Qin amefafanua msimamo thabiti wa China na kutoa madai ya wazi juu ya swala la Taiwan na maslahi na ufuatiliaji wake mkubwa. Qin amedokeza kuwa swala la Taiwan ni kiini cha maslahi ya msingi ya China, ni suala muhimu zaidi na hatari linalokabili uhusiano kati ya China na Marekani. China inahimiza Marekani kufuata kanuni ya China Moja na taarifa tatu za pamoja za China na Marekani, na kutekeleza ahadi yake ya kutounga mkono "Taiwan ijitenge na China".

Mawaziri hao walikuwa na mazungumzo ya muda mrefu yaliyo ya wazi, ya kina na ya kiujenzi kuhusu uhusiano wa nchi hizo mbili na masuala muhimu. Pande hizo mbili zilikubaliana kutekeleza kwa pamoja makubaliano muhimu yaliyofikiwa na marais wa nchi hizo mbili kisiwani Bali, kudhibiti ipasavyo tofauti, na kuendeleza mazungumzo, mabadilishano na ushirikiano.

Pande zote mbili pia zimekubali kudumisha mawasiliano ya hali ya juu. Waziri Blinken amemwalika waziri Qin kufanya ziara nchini Marekani, na Qin ameeleza utayari wake wa kufanya ziara hiyo katika wakati unaofaa.