Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika (UA) Bw. Moussa Faki Mahamat Jumamosi alitoa taarifa akilaani shambulizi la kigaidi lililotokea magharibi mwa Uganda na kusababisha vifo vya makumi ya wanafunzi.
Bw. Faki alilaani vikali shambulizi hilo la kigaidi ambalo linashukiwa kufanywa na kundi la ADF kwenye sekondari iliyoko karibu na mpaka wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) huko magharibi mwa Uganda.
Aidha alitoa salamu za rambirambi kwa familia za marehemu, na kuwatakia wanafunzi waliojeruhiwa wapone haraka. Alisisitiza tena haja ya kuchukua hatua ya dharura ya pande zote, na kukabiliana na tishio la magaidi na makundi yote yenye silaha kutoka DRC, ili kuhakikisha usalama wa kikanda. UA utaendelea kuunga mkono kithabiti serikali na watu wa Uganda.