Shirika la Habari la Qatar (QNA) limesema, nchi hiyo na Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) zimetangaza kurejesha uhusiano wa kidiplomasia.
Kwa mujibu wa Shirika hilo, Ubalozi wa Qatar ulioko Abu Dhabi na ubalozi mdogo mjini Dubai, na pia ubalozi wa Umoja wa Falme za Kiarabu mjini Doha vitafunguliwa jumatatu ijayo.
Pande hizo mbili zimesisitiza kuwa hatua hiyo muhimu inaashiria ari ya uongozi wa nchi zote mbili, na inachangia katika kuendeleza maslahi ya pamoja ya Nchi za Kiarabu na kutimiza matarajio ya watu wa nchi hizo mbili.
Juni, mwaka 2017, Saudi Arabia, UAE, Bahrain na Misri zilitangaza kuvunja uhusiano wa kidiplomasia na Qatar, kwa madai kuwa nchi hiyo inaunga mkono ugaidi na ukosefu wa utulivu katika kanda hiyo, madai ambayo yalipingwa vikali na Qatar.