Waziri Mkuu wa China asema yuko tayari kushirikiana na Ujerumani kwa ajili ya utulivu wa kimataifa
2023-06-20 10:01:10| CRI

Waziri Mkuu wa China Li Qiang Jumatatu alikutana na Rais wa Ujerumani Frank-Walter Steinmeier katika ikulu ya rais huko Berlin, na kuwasilisha salamu za Rais wa China Xi Jinping kwa Rais Steinmeier.

Mwaka jana zikiadhimisha miaka 50 tangu kuanzishwa kwa uhusiano wa kibalozi kati ya China na Ujerumani, Li alisema, Xi na Steinmeier walipeana pongezi na kufanya mazungumzo kwa njia ya simu, na kutoa mwongozo wa kimkakati kwa ajili ya maendeleo yenye afya na thabiti ya uhusiano wa pande hizo mbili.

Amesema China daima inatilia maanani sana uhusiano kati ya China na Ujerumani, akiongeza kuwa ziara yake nchini Ujerumani na kuongoza mashauriano ya saba kati ya serikali za China na Ujerumani na Kansela Olaf Scholz wa Ujerumani, inalenga kutekeleza makubaliano yaliyofikiwa na wakuu wa nchi hizo mbili, kuendelea kuongeza hali ya kuaminiana na kuondoa mashaka, kuchunguza fursa mpya za ushirikiano kati ya nchi hizo mbili, kuimarisha ushirikiano wa pande zote wa kimkakati kati ya China na Ujerumani, na kuchangia maendeleo ya nchi zote mbili na kufufua uchumi wa dunia.

Kwa upande wake, Steinmeier alisema Ujerumani iko tayari kuwa mshirika wa kuaminika wa China ili kulinda kwa pamoja ukombozi wa biashara na kukabiliana na changamoto kama vile mabadiliko ya tabia nchi. Amesema Ujerumani inapinga utengano na aina yoyote ya makabiliano ya kambi, na inapenda kuimarisha mawasiliano na China ili kufanya juhudi za pamoja za kuhimiza amani na maendeleo ya dunia.