Kenya na Umoja wa Ulaya (EU) Jumatatu zilihitimisha mazungumzo ya kisiasa ya Makubaliano ya Ushirikiano wa Kiuchumi (EPA) ambayo yatakuza biashara kwa bidhaa na kutoa fursa mpya za kiuchumi.
Makubaliano hayo yaliyofikiwa Nairobi nchini Kenya, kati ya Makamu wa Rais wa Tume ya Tendaji ya Ulaya ambaye pia ni Kamishna wa Biashara Valdis Dombrovskis na Waziri wa Uwekezaji, Biashara na Viwanda wa Kenya Moses Kuria, yatarahisisha biashara na uwekezaji kati ya EU na Kenya.
Kwenye taarifa yao ya pamoja viongozi hao wamesema linapokuja suala la masharti endelevu kama vile ulinzi wa hali ya hewa na mazingira na haki za wafanyakazi, ni mpango kabambe wa biashara kati ya EU na nchi inayoendelea.
Kwa mujibu wa takwimu, EU ni kituo cha kwanza cha mauzo ya nje ya Kenya na mshirika mkubwa wa pili wa kibiashara, ambapo thamani ya biashara yake katika mwaka 2022 ni jumla ya dola za Kimarekani bilioni 3.6, likiwa ni ongezeko la asilimia 27 ikilinganishwa na mwaka 2018.