Xi akutana na Blinken mjini Beijing
2023-06-20 09:59:18| CRI

Rais Xi Jinping wa China amekutana na waziri wa mambo ya nje wa Marekani Antony Blinken Jumatatu hapa mjini Beijing.

Akibainisha kuwa dunia inaendelea na nyakati zinabadilika, Xi alisema kwa ujumla dunia inahitaji uhusiano tulivu wa China na Marekani, na kama nchi hizo mbili zinaweza kupata njia sahihi ya kupatana inategemea na siku zijazo na hatima ya binadamu.

Xi alisema kuwa Dunia ni kubwa ya kutosha kushughulikia maendeleo husika na ustawi wa pamoja wa China na Marekani. Wachina, kama Wamarekani, ni watu wenye heshima, wanaojiamini na wanaojitegemea, na wote wana haki ya kutafuta maisha bora. Amesisitiza kuwa maslahi ya pamoja ya nchi hizo mbili yanapaswa kuthaminiwa, na mafanikio yao ni fursa na sio kutishiana.

Kwa upande wake, Blinken aliwasilisha salamu za Rais Biden kwa Rais Xi, akisema Rais Biden anaamini kuwa Marekani na China zina wajibu wa kusimamia uhusiano wao kwa maslahi ya Marekani, China na dunia. Ameongeza kuwa Marekani imeazimia kurejea kwenye ajenda iliyowekwa na marais hao wawili huko Bali, na pia inasimama na ahadi zilizotolewa na Rais Biden, yaani kutotafuta vita vipya baridi, kutotafuta kubadili mfumo wa China, miungano yake kutoilenga China, kutounga mkono "Taiwan kujitenga na China", na kutotafuta mgogoro na China.