Tume ya Mpito ya Umoja wa Afrika nchini Somalia (ATMIS) imeanza kuwaondoa wanajeshi 2,000 nchini Somalia.
ATMIS imesema kuwa vikosi vya usalama vya Somalia vilidhibiti kambi ya kijeshi ya Haji-Ali katika Jimbo la Hirshabelle, na kuashiria kuanza rasmi kuondoka kwa wanajeshi hao 2,000 kufikia Juni 30.
Tume hiyo ya AU imesema kuwa kamanda wa kambi ya kijeshi ya ATMIS inayosimamiwa na askari kutoka Jeshi la Ulinzi la Taifa la Burundi Bw. Richard Binyenimana alikabidhi kambi hiyo kwa kamanda wa Jeshi la Taifa la Somalia Bashir Abukar Ahmed katika hafla iliyohudhuriwa na maafisa wakuu wa ATMIS na Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Usaidizi nchini Somalia.
ATMIS pia inatarajiwa kuwaondoa wanajeshi wengine 3,000 ifikapo Septemba kwa kuzingatia Maazimio ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa nambari 2628 na 2670, ambayo yanaiagiza ATMIS kukabidhi majukumu ya usalama katika maeneo yaliyokubaliwa kwa vikosi vya usalama vya Somalia.