Waziri mkuu wa China atoa wito wa kuimarisha zaidi ushirikiano kati ya China na Ujerumani
2023-06-21 09:58:59| CRI

Waziri mkuu wa China Bw. Li Qiang Jumanne alipokutana na Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz alisema, China inapenda kushirikiana na Ujerumani katika kufanya juhudi za kuongeza kiwango cha uhusiano kati ya China na Ujerumani ili kuleta maendeleo zaidi ya nchi mbili, na kuongeza chachu na utulivu duniani.

Li alisema wakati Scholz alipofanya ziara nchini China mwezi Novemba mwaka jana, rais Xi Jinping wa China alifanya naye mazungumzo ya kina, na kutoa mwelekeo kwa maendeleo ya uhusiano kati ya China na Ujerumani katika siku za usoni.

Li aliongeza kuwa zikiwa ni nchi zenye ushawishi, China na Ujerumani zinapaswa kushirikiana zaidi. Tangu kuanzishwa kwa uhusiano wa kibalozi kati ya nchi mbili miaka 51 iliyopita, China na Ujerumani zinaendelea kuimarisha mawasiliano na ushirikiano chini ya moyo wa kuheshimiana na kunufaishana, kuanzisha uhusiano wa wenzi wa kimkakati wa pande zote, na kuhimiza kwa pamoja maendeleo mazuri na ya utulivu ya uhusiano wa China na Umoja wa Ulaya.

Pia alisema kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi ni moja ya wazo la mwongozo la ushirikiano kati ya China na Ujerumani katika siku za usoni. Nchi hizo mbili zinapaswa kuhimiza ushirikiano kwenye sekta za teknolojia ya kijani na viwanda.