Ubalozi wa China kuwakaribisha wanafunzi wa Kenya ili kuimarisha uhusiano wa kielimu
2023-06-22 09:33:46| CRI

Ubalozi wa China nchini Kenya Jumatano ulifanya kikao cha maingiliano na wanafunzi wa Kenya ili kuimarisha ushirikiano katika nyanja za elimu na utamaduni, katika shamrashamra zake za kuadhimisha sikukuu ya Mbio za Mashua ama “Duanwu”.

Hafla hiyo, iliyopewa jina la "Ndani ya Ubalozi, Muulize Balozi," ilileta pamoja wanafunzi kutoka Shule za Upili ya Kenya na Shule ya Upili ya Alliance, ambazo ni sekondari zinazoongoza nchini Kenya.

Balozi wa China nchini Kenya Zhou Pingjian alisema kikao cha maingiliano ni muhimu sana kwa vile elimu na mabadilishano ya kitamaduni yanasalia kuwa msingi wa ushirikiano wa China na Kenya.

Amebainisha kuwa China ina fursa katika nyanja mbalimbali zikiwemo elimu, afya, maendeleo ya teknolojia na viwanda, na kuwataka wanafunzi hao kuendelea na masomo zaidi katika fani hizo nchini China.

Zhou amesema urafiki kati ya China na Kenya una historia ndefu ambayo imeshuhudia maendeleo ya haraka katika mabadilishano na ushirikiano katika nyanja nyingi. Alisema uhusiano kati ya China na Kenya umekuwa ukiimarika na kuwataka wanafunzi hao kuchangamkia fursa ya ushirikiano mzuri ili kutimiza ndoto zao.