Mapigano makali yaendelea kati ya pande hasimu Sudan
2023-06-23 08:25:26| CRI

Mapigano makali kati ya Vikosi vya Jeshi la Sudan na Vikosi vya Msaada wa Haraka (RSF) yaliendelea jana Alhamisi katika maeneo mbalimbali ya mji mkuu Khartoum.

Kwa mujibu wa mashahidi na kamati za upinzani, mapigano hayo zaidi yalifanyika mashariki mwa Khartoum, kaskazini mwa mji wa Bahri (Khartoum Kaskazini), na magharibi mwa mji wa Omdurman. Mapigano hayo yamezuka upya jana karibu na kitongoji cha Burri, huku ndege za kivita zikiruka kwenye anga ya eneo hilo. Aidha makombora ya mizinga yaliangukia sehemu kadhaa za Burri, na majengo ya makazi yaliathirika, lakini hakuna vifo au majeruhi walioripotiwa hadi sasa.

Wakati huohuo jana, Naibu Mwenyekiti wa Baraza la Utawala la Sudan, Malik Agar, alitangaza kwenye Twitter kwamba baraza hilo limekataa mapendekezo yaliyotolewa na Umoja wa Afrika ya kusuluhisha mgogoro wa Sudan, akielezea kusimamishwa uanachama wa Sudan katika Umoja huo.

Agar pia alielezea kutoridhishwa kwake na mpango wa hivi karibuni uliotolewa na Mamlaka ya Maendeleo ya Kiserikali (IGAD), akisema IGAD ilikuwa inataka kuingiza vikosi vya Umoja wa Mataifa nchini Sudan na kuidhoofisha kijeshi Khartoum kupitia "mpango wake wa kuikalia."